WANAKUSUBIRI
Pumzi kali watoa, ishara ya kumaliza,
Nguvu zinakuishia, miguu
unaburuza,
Mengi unajiwazia, kufika utaweza?
Wanakusubiri!
Wanakusubiri wote, wazee pia vijana,
Wanakumezea mate, kwa uchu wanaonana,
Wanasubiri upite, wabaki kuulizana,
Wanakusubiri!
Jirani akusubiri, kushindwa akuwazia,
Mawazoye ya hatari, mashimo kakuchimbia,
Safari yako si shwari, miba kakutegea,
anakusubiri!
Kizee chenye tunguli, kwa hamu kimetulia,
Chajiuliza maswali, vipi kitakuondoa,
Na usiku hakilali, kukuua chawazia,
chakusubiri!
Rafikizo hawapendi, kukuona ukishinda,
Wamekiunda kikundi, kwa visu wanakuwinda,
Wameiandaa gundi, wamekupimia sanda,
Wanakusubiri!
Wakuu wanaumia, vyeo utajawapoka,
Kushinda wamepania, upupu watakupaka,
Kwa waganga wakuendea, kwawe wanaangaika,
Wanakusubiri!
Bibi yako kachukia, zawadi kakwandalia,
Taji ataitumia, ukichaa kukutia,
Kikao kakukalia, penye nia pana njia,
anakusubiri!
Shangazi naye kafura, mate chini kayatema,
Kaburi amelichora, pembe nne utazama,
Ameibadili sura, kwa bidii ajituma,
anakusubiri!
Ni baba na yeye mama, kwa heri wanasubiri,
Mwana wao umesoma, kwa shida nazo hatari,
Matunda watayachuma, mwisho wa yako safari,
Wanakusubiri!
www.kapele h.blogspot.com
Hapo kaka umenishawishi kukipenda kiswahili lakini nakuomba utunge shairi la mwaka 2013 kuusifia Mkoa wa Rukwa maana naupenda sana.very sorry kama nitakukera. I know it's hard task to compose poem but make sure you consider my opinion
ReplyDeleteushairi mzuri
ReplyDeletenapenda kuandika maishairi kwenye blog nifanyeje?
ReplyDelete