Advertise here.

unatangazo? weka hapa

Saturday 28 December 2013

UWANJA WA KISWAHILI Na: Kapele, H

                                                               FASIHI SIMULIZI

M.M. Mulokozi (1996) anasema, Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.

 Baada ya kuangalia maana ya fasihi simulizi yafuatayo ni maaelezo kuhusu chimbuko la fasihi simulizi kupitia nadharia ya ubadilikaji taratibu ambayo itathibitisha kauli isemayo kuwa fasihi simulizi ni masalia ya kazi au sanaa za vizazi vya kale. Kwa mujibu wa Okpewho, (1992) anasema kuwa mwanzilishi wa nadharia hii ni Charles Darwin ambaye anasema kuwa “viumbe hai vyote vimekuwa vikipitia mabadiliko mbalimbali ya muda mrefu hadi kufikia hali hii tuiyonayo sasa”.  Dhana yake hii imeleta ushawishi mkubwa kwa wanataaluma mbalimbali wa fasihi simulizi ambao wanaamini kwamba, fasihi simulizi ni masalia ya zamani au mabaki ya sanaa jadi zilizotangulia kama vile visasili, visakale, ngano, hekaya, methali, nyimbo, vitendawili nk.

Wanaendelea kusema kuwa sanaa hizi zilirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na ziliendelea kupoteza uhalisia wake kadri muda ulivyozidi kwenda. Nadharia hii ilitawaliwa na mbinu ya ulinganishi ambapo walijikita zaidi katika kulinganisha fasihi ya jamii moja na nyingine na katika ulinganishaji wao waliangalia zaidi kipengele cha maudhui kuliko kipengele cha fani.

UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI KATIKA JAMII
Licha ya wanaubadilikaji taratibu kuonesha uhalisia wa fasihi simulizi kuwa ni masalia ya kazi za kale au mabaki ya zamani, hoja hii haimaanishi kwamba fasihi simulizi haina thamani au uamilifu wowote katika jamii ya leo lahasha! Hivyo tunaungana na wanasosholojia ambao wanasisitiza kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai ila unabadilika tu kulingana na maendeleo ya jamii husika na dhima zake zinatawala masuala mtambuko kama ifuatavyo:

Kuburudisha; tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hutumika kama nyenzo ya burudani katika Nyanja mbalimbali za kijamii. Mfano wa tanzu hizo ni kama vile hadithi, ushairi (nyimbo mbalimbali), semi (methali, vitendawili). Tanzu hizi hutoa burudani katika sehemu mbalimbali, mfano nyimbo, zipo nyimbo ambazo hutumika kutoa burudani katika sehemu mbalimbali kama vile harusini-nyimbo za harusi, nyimbo za nyiso hutoa burudani jandoni na unyagoni. Vilevile katika siasa zipo nyimbo ambazo hutumika kutolea burudani na uhamasishaji wakati wa kampeni za kisiasa. Hivyo basi kutokana na utanzu huu wa nyimbo kutumika kama chombo cha burudani katika Nyanja mbalimbali huonesha dhahiri kuwa ni kwa namna gani fasihi simulizi inavyojitokeza katika masuala mtambuko.

Kuelimisha; kupitia fasihi simulizi jamii hujipatia elimu ambayo huwasaidia kuijua vizuri historia yao, utamaduni, siasa ya nchi yao pamoja na itikadi. Mfano katika historia zipo kazi za fasihi simulizi ambazo huonesha historia, kazi kama utenzi wa Fumo Lyongo, utendi wa Shaka Zulu ambao hutupatia historia na utamaduni wa watu wa Afrika kusini. Pia ndani ya tendi hizo kuna masuala ya uongozi pamoja na siasa. Vilevile zipo methali ambazo huelimisha watu kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea nafasi yao kiuchumi, kwa mfano; “mgaagaa na upwa hali wali mkavu”. Kadhalika katika upande wa afya zipo methali zinazotoa elimu mfano “kinga ni bora kuliko tiba”. Hivyo basi utoaji huo wa elimu katika Nyanja tofauti tofauti huonesha ni kwa namna gani fasihi hii ilivyokuwa inajihusisha na masuala mtambuko ya kijami.

Kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii; katika suala hili pia fasihi simulizi haikuwa nyuma kwani zipo kazi mbalimbali ambazo hutumika kama nyenzo kuu na muhimu za kuhifadhia amali za jamii kwa mfano visasili na visakale hutunza historia na utamaduni wa jamii husika, mfano; kisasili cha kibo na mawenzi hutunza historia ya Tanzania kuhusu mlima Kilimanjaro. Pia zipo methali ambazo hutunza utamaduni wa waafrika hususani Tanzania mfano; “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”, methali hii hutunza utamaduni wa kiafrika kuwa wadogo lazima wawasikilize na kuwaheshimu wakubwa. Kadhalika katika siasa kupitia kipera cha lakabu ya baba wa taifa huonesha historia ya kiongozi wa Taifa la Tanzania. Na hivyo ndivyo namna fasihi simulizi inavyojihusisha na masuala mtambuko.

Kuhamasisha umoja na mshikamano; suala hili pia hufanywa na aina hii ya fasihi simulizi katika jamii na hujidhihirisha katika Nyanja mbalimbali kama vile siasa, zipo methali ambazo uhamasisha suala hili:- “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”, “Kidole kimoja hakivunji chawa”. Kwa upande wa nyimbo zipo pia ambazo huhamasisha suala hili kama vile nyimbo za chapuzo mfano; wawe-kilimo, kimai-uvuvi. Vileveli zipo nyimbo ambazo huhamasisha umoja na mshikamano wakati wa michezo.

Kukuza lugha; fasihi simulizi hujikita pia katika suala hili la ukuzaji lugha kupitia vipera mbalimbali ambavyo hufanyika katika nyanja mbalimbali kwa mfano nyanja ya elimu, vipo vipindi mbalimbali redioni na hata kwenye luninga ambavyo hutumika kufundishia lugha hasa kwa watoto kwa kupitia vipera vya fasihi simulizi kama vile vitendawili na methali, zipo pia chemshabongo na hadithi mbalimbali. Vilevile ipo michezo ya watoto ambayo hukuza lugha kama vile kauli tauria, mfano; “Katibu kata wa kata ya mkata alikataa katakata kukata miti katika kata ya mkata”. katika siasa uibukaji wa misimu mfano, chakachua, ngangari nk. pamoja na nyimbo hasa wakati wa kampeni husaidia kukuza lugha. Pia shughuli mbalimbali za kijamii mfano harusi, misiba kupitia nyimbo za watani pia hutoa mchango mkubwa katika kukuza lugha.

Kuonya na kukosoa jamii zipo tanzu na vipera mbalimbali vya fasihi simulizi ambavyo hujihusisha zaidi na kuiweka jamii katika nafasi iliyobora zaidi. Mfano; kimaadili kuna methali zinazoonesha maadili mema katika jamii mfano; “Samaki mkunje angali mbichi”, “Mkaidi hafaidi mpaka siku ya iddi”. Vilevile kiuchumi zipo methali ambazo huonya na kukosoa wale wote wenye tabia za kivivu katika kujitafutia maisha mfano, “Mtegemea cha ndugu hufa masikini”, “Fanyakazi kama mtumwa uishi kama mfalme”.

Vilevile kuongeza kipato; kupitia fasihi simulizi watu hujiajiri na kujipatia kipato. Kwa mfano; watu hujishughulisha na utanzi wa nyimbo mbalimbali kama vile nyimbo za kisiasa, kiuchumi pamoja na nyimbo za kiutamaduni ambapo kwa namna moja au nyingine huwasaidia katika suala zima la kujipatia kipato na kusukuma mbele gurudumu la maisha kwa ujumla.


Masuala mtambuko ni mambo yanayojitokeza katika Nyanja mbalimbali za kijamii, kwa mfano magonjwa, rushwa, ufisadi nk. Mfano wa Nyanja hizo ni kama vile siasa, uchumi, utamaduni na jamii kwa ujumla

TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila (2003).

Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo, vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)


Tanzu hizi za fasihi simulizi huweza kuwekwa katika kumbo au michepuo yake. Bali upo utata katika kuainisha kumbo hizi, utata huu uanasabishwa na kutokuwepo kwa nadharia teule ambazo zingeweka wazi njia au vigezo muhimu ambavyo vingefaa kutumika katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi. Katika kutalii uwanda wa fasihi simulizi wataalamu wengi wanatumia vigezo vya maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika, na namna ya uimbaji. Hebu tuyatalii mawazo ya watalaamu hawa na uainishaji wa kumbo za fasihi simulizi.

Mulokozi (1996), mtaalamu huyu yeye anajaribu kuainisha tanzu sita za fasihi simulizi ambazo ni:
a.      semi
b.      mazungumzo
c.       masimulizi
d.      maigizo
e.       ushairi
f.       ngomezi
Ndungo na Wangali, wao wanazianisha tanzu tano za fasihi simulizi wanaanza na:
a.      hadithi
b.      ushairi na nyimbo
c.       sanaa za maonesho
d.      methali
e.       vitendawili
wataalamu wote wanamitazamo inayoendana katika kuainisha tanzu za fasihi simulizi, baada ya kutambua mawazo yao sasa ni vema kutumia nafasi hii kuziweka tanzu hizi katika makundi jumuishi manne ambayo ni:
a.      sanaa za maonesho
b.      semi
c.       masimulizi
d.      ushairi

tanzu hizi zinahusiana katika kukamilisha utendaji wa fasihi simulizi na ili kujadili vema ni vema tuanze na mchepuo wa semi.

SEMI
Ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Katika kuainisha utanzu huu vipo vigezo kama vile kigezo cha lugha na kigezo cha dhima ambacho kujifunza.Tanzu au kumbo hili lina vijitanzu vyake vinavyotumika katika kuweka uhai wake, nanvyo ni:
a.      methali
b.      vitendawili
c.       mafumbo
d.      misimu
e.       lakabu
f.        kauli- tauria
Baada ya kujua vijitanzu vya utanzu wa semi sasa ni vizuri kuanza kujadili kijitazu cha kwanza ambacho ni methali, katika kijitanzu hiki tutajadili maana, chimbuko, umiliki, uwasilishaji, muundo, mitindo, sifa, na umuhimu wake kwa jamii.

 METHALI

Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii, au ni maneno ya hekima na busara ambayo hutolewa na mtu mmoja na baadaye maana ya maneno hayo hutolewa. Jambo la msingi katika kutoa maana ama fasili ya methali ni kuangalia mazingira. Pia methali ni usemi mfupi wa mapokeo ambao hudokeza kwa ufupi tajiriba ya jamii fulani.

Chimbuko la methali
methali zinatokana na:
a.       visasili, mfano nyama ya ulimi huponya imetokana na masimulizi ya Kiswahili yaliyomuhusu mfalme.
b.       maoni na uzoefu Fulani wa kihistoria mfano keshokesho haikumuua mzungu.
c.       Uchunguzi wa vitu katika mazingira, tabia na mienendo ya watu katika jamii. Mfano, moto hauvukwi mara mbili. Methali hii huimiza utendaji.

Umiliki wake
Methali kama kijitanzu cha semi humilikiwa na jamii nzima hata kama ilitolewa na mtu mmoja. Kwa ufupi twaweza kusema kuwa ni mali ya jamii nzima.

Uwasilishaji wake
Uwasilishaji wake hutegemea zaidi unaongea na nani? Unaongea nini? mfano unaongea katika mazungumzo rasmi kama vile hotuba, ibada au risala.

Muundo wake
Methali huundwa kutegemea jamii moja na nyingine na aina ya maudhui. Mfano methali ya swali, mavi usiyala wayawangiani kuku?
                 Mla mla leo mla jana kala nini?
                 Pilipili uso ila yakuwashia nini?

                 Methali muundo wa sentensi
a.       masikio hayazidi kichwa
b.      mkate makavu wa nyumbani ni bora kuliko nyama ya shuwa yap engine.
c.       Kata pua uunge wajihi
d.      Mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani
e.       Mwenda kwao si mtoro.
f.       Mwenda kwao haogopi giza.



                    Mtindo wa methali
Katika mitindo ya methali yapo mambo muhimu yaliyoingizwa miongoni mwa mambo hayo ni:

  1. Sitiari zimeingizwa zaidi. Mfano ukiona vyaelea jua vimeundwa, mgeni ni kuku
      mweupe.
  1. mirudiorudio ya silabi au sentensi. Mfano ukiujua huu, huu huujui, hayawi hayawi huwa.

SIFA ZA METHALI
Methali zina sifa zifuatazo:
i.                    zinaufupisho wa maneno
ii.                  zina muundo wa kishairi.
iii.                Huingiza lugha ya
iv.                Hujulikana na jamii nzima
v.                  Huwa na pande mbili (nyingi)

Katika kujadili sifa za methali mtaalamu mmoja amejaribu kuzigawa methali katika makundi manne (4), ambayo ni:

i.                    Methali za imani ya binadamu kwa Mungu. Mfano, muumba ndiye muumbua, Mungu ndiye muumba, kalamu ya Mungu haikosi.
ii.                  Methali zinazo taja binadamu na viungo vyake. Mfano, hawi Musa kwa kuchukua fimbo, ugeni ni utoto, usiwe na kucha ndefu.
iii.                Methali zinazotahamini matendo na tabia za watu (hujenga tabia njema) mfano asiona nafsiye haoni akioneshwa.
iv.                Methali zinazotaja mambo au matendo mbalimbali yanayotokea mara kwa mara na kuathiri maisha ya binadamu. Mfano, mtenda mema kinyuki jaziye hulipwa mema, kenda fumbata si kumi nenda rudi, ndege aliyemkononi ni bora kuliko kumi walio mtini, ajali inasababu.

 UMUHIMU WAKE KATIKA JAMII
i.                    Methali huelimisha jamii,
ii.                  Methali huonya na kuhasa jamii
iii.                Methali hukuza uwezo wa kufikiri ( hufikirisha)
iv.                Methali hutunza amali za jamii husika.
v.                  Methali hujenga mahusiano mema.

Methali ni utanzu unaotegemea sana fani nyingine ili uweze kukua na kuenea, mfano maongezi au majadiliano mazito. Pia kipera hiki na ni sanaa elezi kwa hutumiwa kufafanua na kukazia jambo linalozungumzwa ili ieleweke vizuri. Mwisho methali inaweza kuwa na umbo au mtindo wa kishairi, mfano haba na haba hujaza kibaba.

VITENDAWILI
Kama ilivyo katika methali utaratibu uliotumika kufafanua kipera methali utatumika pia katika kufafanua kipera vitandawili.

 Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo. Pia vitendawili ni semi fupi zenye kuwakilisha maana pekee za vitu, vitu vinaweza kuwa kimazingira au kitabia, vilevile zinahitaji kuwa na maana sahihi za kifasihi. Mteguaji anatakiwa ategue kifasihi na apate dhana inayotegemewa.

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA VITEDAWILI
i.                    Tatizo la kutatuliwa. Kanuni ya utangulizi inapoanzwa.
ii.                  Kitendawili si kitendawili hadi kiteguliwe. Hivyo jibu ni sehemu ya kitendawili mwanzo wa kifomula, majibu na hatua zote zinazofuata na majibu yanaposhindwa kuteguliwa ni kitendawili. Mwanzo hadi mwisho ni kitendawili, kila hatua ni sehemu ya kitendawili.

Uainishaji
Fani na maudhui kifasihi hutumika. Uainishaji wowote ule hutegemea vitu fulani katika maudhui kuna ujumbe, dhana…

Maudhui ni jumla ya mambo yote yanayosemwa katika maandishi ama ktaika mazungumzo.

Fani hushughulika na kwa vipi kitu ama maudhui yanavyosemwa au kuwasilishwa. Mtindo, wahusika na mtindo. Vifuatavyo ni vigezo vya uainishaji wa vitendawili.

  1. Tukio au jambo. Katika kuelezea kigezo hiki watu, wadudu, mimea, teknolojia,
      mila na desturi huusika. Mfano miti yote nipanda lakini mtalawanda utanishinda.
      Jibu: huwezi kumuoa dada yako.

  1. Urefu. Kuna urefu wa aina mbili: mpumuo – moja (maelezo mafupi) mfano nyumba yangu haina mlango. Jibu yai, mpumuo- mwingi/ mrefu. Mfano kulikuwa na mama alikuwa na watoto warefu…lakini bado kunautata katika vigezo hivi vya vitendawili. Hivyo basi ni vema kikatumika kigezo cha ugumu au utata pamoja na kile cha urahisi katika kuainisha vitendawili.
                   
                        VITENDAWILI TATA (SIFA)
i.                    huanza na kanuni.
ii.                  Huwasilishwa kwa maneno yenye mtiririko na maswali.
iii.                Hufunguliwa na akili na uwezo mkubwa.
iv.                Huwasilishwa…


                                  VITENDAWALI RAHISI (sifa)
           
       i .       huanza na kanuni ama fomula.
     ii.         ni sentensi wala si swali.
iii.                ni vya moja kwa moja na hueleweka moja kwa moja.
iv.                Hutegwa kwa urahisi kutegemea mkitadha na kunga za vichekesho na kishairi.


MTINDO AU MBINU ZA VITENDAWILI

Kuna mitindo mingi ya vitendawili kama ifuatavyo:
·         Onomatopia (matumizi ya sauti ) mfano prii mpaka maka, fu funua.
·         Mbinu ya kishairi, mpango wa maneno na mapigo ya kimziki. Mfano
            futika futika futikafutika.
·         Matumizi ya nafsi na uhaishaji. Mfano popoo mbili zavuka mto
·         Matumizi ya kejeli. Mfano kitu kidogo kimemtoa mfalme kitini.
·         Matumizi ya tashbiha. Mfano msichana mdogo anapika vizuri kuliko mama yake- nyuki. Babu mfupi anamwangusha babu mrefu- shoka

UWASILISHAJI

Uwasilishaji wa vitendawili unategemea sana uwepo wa pande mbili ambazo ni: mtegaji- anayetoa, mteguaji- anayejibu. Kuna mabadilishano na hakuna hadhira katika uteguaji. Katika baadhi ya makabila wazee wanaweza kuwa hadhira kabla ya kutega huanza na tangazo. Mfano tutaanza kutega na kutegua vitendawili.

KWA NINI KANUNI KATIKA VITENDAWILI

Kuna umuhimu mkubwa wa kufuata kanuni katika vitendawili, na umuhimu huu ni kama ifutavyo:
i.                    Kuandaa utayari kiushindani.
ii.                  Kuwatoa washiriki katika shughuli zao na kufuata mukitadha wa kiutendawili
iii.                Huwafanya washiriki kuwa makini ….
iv.                Kufafanua na kuainisha mtegaji na mteguaji katika kundi.
v.                  Huwajulisha kitendawili kinachofuata. Kwa kawaida vitendawili hutolewa na watoto au ni vya watoto. Lakini haina maana kuwa watoto ndio wahusika wakuu. Mara nyingi hutegwa usiku. Kwa sasa vitendawili husomwa shuleni, mukitadha wa vitendawili umebadilika kutokana au kulingana na mabadiliko na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuhama kwa vitendawili hubadulika maana.

UMUHIMU WAKE
i.                    kufikirisha
ii.                  kujenga umoja
iii.                kukuza na kuitunza utamaduni

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UCHAMBUZI

  1. Muda au wakati ( muda gani kilitegwa na sasa kinategwaje)
  2. Mazingira. Mfano kuku wangu katagia mwibani- nanasi. (zingatia mazingira)
  3. Maana na jibu litolewe. Mfano kaburi la mfalme lina milango miwili.
  4. Matumizi ya lugha. Mfano chaka langu halina ubaridi. Ili kuelewa dhana za vitendawili tambua mazingira, silka, na utamaduni wa watu.





Swali muhimu.

Vitendawili ni fasihi ya watoto, hivyo ni kupoteza muda kuvisoma katika mihadhara ya chuo kikuu. Jadili.




                                Dondoo za ujibuji.
i.                    utangulizi
-          maana ya vitendawili
-          sifa za vitendawili
-          uwasilishaji wa vitendawili
-          sifa za vitendawili
ii.                  kiini
-          umuhimu wa kusoma vitendawili kama kipera cha semi katika fasihi simulizi.
iii.                hitimisho
- mambo ya kuzingatia katika uchambuzi wa vitendawili.

MAZUNGUMZO
Mazungumzo ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Mfano wazungumzaji wanaweza kutumia lugha ya makato, methali,vitendawili, nahau, na tamathali za semi katika kuzungumza kwao. Matumizi ya lugha ya kisanaa katika mazungumzo hufanaya mzungumzo yakawa utanzu wa fasihi simulizi. Mazungumzo kama utanzu wa fasihi simulizi una vyake vipera ambavyo ni: hotuba, soga, malumbano, mawaidha na ulumbi.

Hotuba; haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao rasmi au mikutano.

Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.
Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.
Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.

Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.

Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.

SANAA ZA MAONESHO – UTANZU WA FASIHI SIMULIZI

Ni maigizo ya fasihi simulizi, maigizo haya huusisha mambo ya dhati ya kutoka kwenye hali zao halisi katika mapito ya maisha na kurudiwa kimchezo na vikundi vya waigizaji. Katika maonesho lazima mtu aone lakini matendo huboresha zaidi. Fasihi simulizi ni halisi ya mwafrika. Ingawa utanzu huu una mambo ya dhati una vipera vyake kadhaa ambavyo ni: majigambo,maigizo, tambiko, miviga, michezo ya watoto, utani, ngonjera, ngomezi vichekesho na michezo ya jukwaani. Vipera hivi vyaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:

MICHEZO YA WATOTO
Michezo hii hufungamana na utamaduni na siasa ya jamii, ni msaada kwa watoto kujifunza mambo ndani ya jamii. Washiriki ni watoto wenyewe, hata kama mtoto yuko peke yake huumba wahusika wake akilini. Mfano mtoto kuongea peke yake katika mchezo fulani. Pia watoto wengi hucheza michezo inayozuka katika jamii yake. (kuiga, kutenda, kuona). Kisayansi ubongo wa watoto huzaliwa ukiwa wazi na kila apokeacho ni sahihi. Michezo hii huchezwa popote na kila mchezo huwa na shabaha na watoto huiga utamaduni wao na vifaa vinavyotumika ni vile vinavyopatikana ndani ya jamii.

LENGO AU MADHUMUNI
i.                    kuburudisha.
ii.                  Kuelimisha/kufunza.
iii.                Kuonesha utamaduni.

TAMBIKO
Ni sadaka kwa Mungu, miungu au mahoka kulingana na jami. Kwa nini tambiko: kuomba (mvua, magonjwa), kushukuru. Katika tambiko yapo mambo muhimu yanayofanya tambiko liwe miongoni mwa vipera vya sanaa za maonesho mambo hayo ni:

i.                    uwanja wa kutendea, mfano: miti mikubwa, njia panda, kaburi na misitu minene.
ii.                  Maleba, hivi ni vifaa maalumu ambavyo hutumika katika matambiko, mfano: ngozi, mashuka, mgwishu, kisu, kibuyu.
iii.                Lugha maalumu. Katika matambiko kuna lugha maalumu inayotumika., lugha hii ni lugha ya unyenyekevu, utulivu na yenye utofauti mkubwa.
iv.                Utendaji katika tambiko, huwahusisha viongozi, wafuasi na dhamira. Vitu hivi hutendwa na kuzungumzwa.

MAIGIZO
Maigizo ni michezo inayotumia watendajikuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine. Lengo kubwa ni kuburudisha na kutoa ujumbe. Maigizo ya kiafrika kama vile maigizo ya watoto, maigizo ya kidini, maigizo ya msibani huambatana   na:  a. ngoma
  1. hadithi
  2. nyimbo
  3. matendo ya kimila
  4. utambaji.

MIVIGA/ JANDO NA UNYAGO
Haya ni mafunzo yanayomfanza mtu namna gani aweze kutenda yeye kama mtu mzima. Unyago ni ngoma ya kumfundisha mwali katika jamii yake. Pia ni taasisi rasmi kama taasisi nyingine. Miviga hii ina zake sifa ambazo ni:

i. utendaji, unaohusisha ngoma na nyimbo.


MAJIGAMBO
Ni kujifanya unajua sana, kujinata na kujivuna. Sanaa iliyokinyume na majisifu mara nyingi katika shairi na masimulizi, mambo makuu na matukufu aliyowahi kuyafanya mtu fulani na mara nyingi sifa za kiumeni hutumika, kuchezwa ngomani na katika masuala ya kiserikali na waimbaji hutumia zeze.

UTANI
Mila ya utani imeenea sana Afrika. Watu wanao taniana kwa maneno na matendo, masharti huzingatiwa. Malumbano ya utani yapo katika michepuo mingi kama ifuatavyo:
i.                    utani wa babu, bibi na wajukuu.
ii.                  Utani wa mashemeji.
iii.                Utani wa makabila.
iv.                Utani wa marafiki.

                        MASIMULIZI

Masimulizi; hii ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha muundo, mara nyingi masimulizi huwa na muundo.
 katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.


Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vilevile kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji. Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalum.

Masimulizi yamegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisalua (kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano.

Ngano (vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha. Pia ngano ni masimulizi ya kubuni yenye kutoa mifano ya binadamu na matatizo yake ulimwenguni na akili ya binadamu kutatua matatizo ili maisha yawe bora zaidi japo kwa muda mfupi hapa duniani. Mafano wa ngano ni pamoja na abunuasi, sungura. Tena masimulizi haya husisitiza kuwa binadamu wajinga au legevu wasiopenda kutumia akili katika kutatua matatizo hufikwa na matatizo na wakati mwingine hufunzwa na ulimwengu. Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.

Dhamira kuu ya ngano huwa ni maisha, kuelimisha roho mbaya, kutia moyo. Ngano hizi kwa kawaida huwa na kianzio na kiitikio chake. Mfano, kianzio chaweza kuwa paukwa/hadithi!hadithi!, pia kiitikio chake chaweza kuwa pakawa, au hadithi njoo! Utamu kolea.

Maudhui katika ngano yanaweza kujikita katika mambo yafuatayo:
-          binadamu wajinga hupata shida.
-           Utamaduni wa jamii husika huonekana katika ngano.
-           Binadamu anaweza kufanya vitu visivyowezekana katika dunia halisi.

WAHUSIKA KATIKA NGANO
Wahusika katika ngano wanaweza kuwa:
  1. binadamu tu
  2. binadamu na wanyama.
  3. Binadamu na pepo.
  4. Binadamu na zimwi.
  5. Binadamu na miti au mawe.
Uhusika mkuu ni wa binadamu kwa yeye ndiye anayepata funzo. Katika muktadha watoto au watu wazima ambao huchorwa tofauti, mfano mdogo wa umbo akili nyingi. Katika hadithi wanyama hutumika kukejeli na kuelezea uovu. Mfano:
i.                    kinyonga – mtu mwenye tabia ya kubadilika badilika.
ii.                  Simba- mtu mwenye nguvu.
iii.                   mkizi- mtu mwenye tabia ya kulala sana na asiyetambua lolote.  Wanyama wadogo huwakilisha wanyonge lakini hushinda.


USIMULIZI WA NGANO
Usimulizi au masimulizi ya ngano huwa ni changamano na huweza kuwa wa moja kwa moja na kueleweka kwa maudhui kwa tegemea sana mwanzo hadi mwisho wa hadithi. Nyimbo, mahojiano, na ngoma hubeba maudhui ya hadithi.

FANI YA NGANO

Fani ni namna mambo au maudhui yanavyosemwa na msimulizi au mwandaaji wa maudhui. Katika ngano fani hujikita zaidi na matumizi ya:
Taswira, jazanda, tashibiha, chuku sambamba na tanakali sauti ambazo huzua picha akilini mwa msikilizaji. Taswira inapokosekana wasikilizaji hupotelewa na mkondo wa hadithi na kushindwa kuunganisha vitushi. Sifa yake kuu ni kwamba huwa fupi na kufanya kusikika vizuri au rahisi.

VIPERA VYA NGANO
Ngano na vipera vyake ambavyo ni:
1. NGANO

ISTIARA: hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Kwanini mafumbo ilikuepuka migogoro baina ya mtunzi ama msimulizi wa hadithi hiyo na wanajamii wanaoweza kuhisi kuwa masimulizi hayo yanawagusa ama kuwahusu kabisa. Mfano kusadikika.

MBAZI: hii ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima. Mfano mzuri ni hadithi ya Binti na Chura.

KISA: hii ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima. Na mara nyingi lugha yake huvutia.
                

2. VISAULA/ HADITHI ZA KIHISTORIA

Ni hadithi zenye kutoa historia lakini si zote huwa za kweli nyingine hubuniwa. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.


VISAKALE/visakalo: haya ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa. huchanganya chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.

MAPISI: haya ni maelezo ya kihistoria bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli. Mfano miradi bubu ya wazawa.

TARIHI: haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.

KUMBUKUMBU: haya ni maelezo ya matukio muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambao ni watu.


VISASILI: hiki ni kipera kinachofungamana na imani za dini na mizungu ya kijamii, pia hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.

VISAINI: haya ni masimulizi ambayo hueleza viini au chimbuko la watu fulani, chanzo cha matukio yanayokanganya akili ya binadamu. Mfano: kifo, kuzaliwa, pia husimulia mambo ya ajabu na imani za kidini na jamii husika. Visaini hivi vinafafanua kuwa kifo ni adhabu toka kwa Mungu tena hupunguza huzuni na kuvikubali vifo.

3. KHURAFA/KHARAFA/HURAFA

Hizi ni hadithi ambazo wanyama wamehusishwa zaidi/kwa wingi na kupewa tabia za wanadamu, huwakilisha vitendo na lugha za binadamu. Mfano: sungura, simba, fisi na kobe. Katika hadithi hizi fanani huongea bila kuudhi watu au hadhira. Hivyo yampasa kutumia lugha mficho ndani ya wanyama ili hadhira wasitambue nani anayesemwa. Umuhimu wa masimulizi haya ni kuwa huifadhi utamaduni wa jamii. Ulimwengu wa wanyama katika kharafa ni ulimwengu halisi wa binadamu. Na kawaida yake wanyama wadogo huwashinda wakubwa.

4. HEKAYA

Hizi ni hadithi ndefu kiasi ya mapokeo yenye kuzingatia matukio machache ya kusisimua na kustajabisha. Inatambulika kwa ujanja wa muhusika mkuu. Aghalabu muhusika anaweza kuwa mtu ama mnyama. Muhusika mkuu hujikuta katika mikasa mingi ni kana kwamba ulimwengu mzima umejaa mikosi na kuonesha kuwa atangamia, hadi mwisho wa kisa ndipo kwa maajabu kabisa aweze kuibuka mshindi na hii huifanya hadithi kuwa na taharuki. Mfano: kisa cha bwana MSA, mzimu wa watu wa kale. Hadithi hizi za hekaya ni visa vingi lakini muhusika ni mmoja. Mfano ABUNUASI, huko Ghana hadithi za aina hii huitwa ANANSE, Afrika zinaitwa BUIBUI, na huko Nigeria zinaitwa KOBE
dhamira kuu ni kuhimiza watu wasife moyo na funzo katika hekaya ni kwamba ukubwa si hoja katika ulimwengu wenye matatizo. Ukubwa wa akili ni ufunguo wa maisha.

5. MIVIGHA
Ni hadithi ambazo zikitiwa katika mizani ya kisayansi, kihistoria na kiamumbile hazioneshi ukweli wowote. Waliozitunga huisisha na vizazi vyao vichanga na matukio hayo huonekana na kuaminika kuwa ni kweli yalitokea. Hadithi hizi huusu chimbuko la kabila ambapo huamini kama kuna mwanzilishi na watu wote huwa wana wa huyo. Huonesha imani ya watu katika jamii, inaambatana imani na itikadi katika jamii.



6. MIGHANI
Ni hadithi zinazohusu mashujaa, mashujaa hao huwa ni wa kitaifa na hustawi sana. Na huitwa majagina au jagina. Hushughulikia sana haki za watu na huwa watu wema. Huwa na wakinzani wao hao huitwa majahili/jahili wao hawajali maslahi ya wengi, makatili, wakandamizaji na katika hadithi hizi mpaka kati ya ukweli wa kihistoria na kibunifu hautambuliki, mpaka sasa jamii zinaamini. Kunapokuwa na mapambano…..

Sifa za mighani:
i. Zina mfumo wa kimaigizo.
ii. Zinatumia ishara.
iii. Zinatumbuiza.
iv. Zinaufaraguzi wa maneno.
v. Zina mwisho maalumu.
vi. Kuna kuwa na fanani.
vii. Kuna utendaji.
viii. Huendana na mazingira.

NADHARIA
Kuna nadharia nyingi zitumikazo katika fasihi simulizi nazo ni:

i.                    Nadharia ya mgeuko/ mabadiliko.
Nadharia hii na waasisi wake hudai kuwa fasihi simulizi huakisi fani ya wakati husiku. Asili ya binadamu ni sawa jamii zote, jamii hizi zina maendeleo yanayofanana hata kama mazingira ya kijiografia yanatofautiana. Msimamo wao wanamabadiliko ua mgeuko wanadai dhana ya kimsingi inayounganisha tamaduni zote zinafanana, vionjo, ubunifu wa mawazo au fikra na imani. Hadthi moja inaweza kusimuliwa jamii moja pia na jamii nyingine kwa utofauti.

ii.                  Nadharia ya msambao.
Hii ni nadharia ambayo wanamsambao wanasisitiza mahusiano yaliyopo kati ya jamii tofauti kwa kuthibitisha kuwa kuna mahusiano ya kijiografia na kihistoria. Hadithi zinafanana katika kila jamii. Zote bila mawasiliano yoyote. Na hadithi husimuliwa kulingana na utamaduni husika. Waasisi wa nadharia hii ni THEODOR BENFEY, EMMANUEL COSQUIN, JULIUS, KEARLE KROHN. Wanamsambao husisitiza zaidi uhainishaji na muundo wa…..ni jamii yenye mfumo wa mawazo aina moja na si mkinzano wa mawazo.

iii.                Nadharia ya kiutendaji.
Katika nadharia hii kuna waasisi kama vile Bron Slawn, Malinowski, Raddife Brown. Wao wanadai kuwa shughuli za kiutamaduni huzingatia falsafa ya jamii. Jamii huchota masimulizi katika desturi, imani, ibada na zimeegemea katika muundo zilizojiwekea.

iv.                Nadharia ya utendaji mpya.
Waasisi wake ni Raymond Firth na Edmund Leach. Wao wanadai kuwa jamii haina muundo mmoja bali siku zote inamafarakano. Katika mtazamo wao jamii haiwezi kuzuia mafarakano. Ili jamii iweze kukua lazima mafarakano yawepo, hakika jamii haiwezi kuwa sawa.




v.                  Nadharia Umbuji.
Mwasisi wake ni Vladimir Prop. Yeye anadai kuwa kuna mahusiano ya masimulizi na wahusika katika kutengeneza msuko au mtiririko. Na anangalia jinsi hadithi zinavyoingiliana katika msuko, mpango na utaratibu.

vi.                Nadharia ya Umuundo
Mwasisi wake ni Cloude Levi, yeye anadai kuwa utamaduni unajumuisha vitu vinavyofanana alichunguza visasili na kusema vinatumika kuelezea na kutatua matatizo. Visasili ni hadithi za kweli zinazoelezea falsafa ya jamii husika na vinahusika na maisha ya jamii.



UAINISHAJI WA MASIMULIZI

Masimulizi yanaweza kuainishwa kama ifuatavyo:

i.                    Kimtiririko, msambao wa masimulizi kijiografia na kihistoria. Mfano hadithi za vitu, matambiko/ibada, kuanguka kwa shujaa.

ii.                  Kimaudhui, zinagawa masimulizi kulingana na ujumbe ndani ya hadithi.
a.       Visasili vya imani za kishirikina, imani za kidini kitamaduni. Mfano asili ya mtu na vitu.
b.      Ngano na Hekaya, ni masimulizi ya kihistoria na kumbukumbu za mashujaa.
c.       Ubunifu na kufikirika, istihala hekaya za kufunza, maadili ngano fupi za kubuniwa, kauli za uongo na za kubuni, hadithi za mafumbo. Ngano, hekaya, visasili zinasimuliwa kuwa ni hadithi za kweli na hazibadiriki.

iii.                Kijamii, zina makundi yafuatayo:
a.       kisiasa, mahusiano ya uongozi na
b.      kiukoo, zinahusu muundo wa familiya fulani. Mfano, ndoa.
c.       Kidini, kunakuwa na uwepo wa mvua.
d.      Kimaadili, ulafi, ujinga,kukosa mtazamo, wizi.
e.       Kiuchumi, kuchukua na kukopa.

iv.                Tabia, zinahusu muhusika mkuu katika hadithi. Mfano visa janja.
a.       hadthi za binadamu, muhusika-binadamu.
b.      Hadithi za wanyama, muhusika-mnyama.
c.       Hadithi za mizimu, muhusika-mzimu.
d.      Hadithi za jinamizi, muhusika-jinamizi.
e.       Hadithi za miungu, muhusika- matukio ya kiungu na miungu.
f.       Hadithi za vitu visivyo na uhai- miti, mawe.

V.                kiutamaduni, unagawa masimulizi kuhusu kujamii na kiutamaduni,
                     lakini pia uainishaji wake unahusu….


MUUNDO NA MTINDO WA MASIMULIZI
Kaka suala la uwasilishaji yapo mambo muhimu ya kuangalia ni nani, wapi, kwa vipi hadithi inasimuliwa. Kuna mitindo todauti ya masimulizi lakini kuna mfanano wa mwanzo-kati-mwisho.

Mwanzo- mwanzo wa hadithi una kanuni zinazofuatwa na kiala jamii ina mwanzo wake. Mfano katika Kiswahili mwanzo waweza kuwa hadithi! Hadithi! Pia paukwaa!
iv.                msimulizi na wasimuliwaji
v.                  mahali au jukwaa la masimulizi.
vi.                Muda au wakati usiingiliane na shughuli nyingine za uzalishaji mali.
vii.              Urefu wa hadithi.
viii.            Shughuli na mipaka yaa uwasilishaji. Hadhira ina amini nini na kwa wakati gani, kwa nini hadithi hazisimuliwi mchana? Hadithi hutegemea sana ujumi wa jamii husika.
Usimulizi wenyewe, katika kipengele hiki kuna msimulizi, masimulizi na hadhira.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.

Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;
Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji, muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada, kilio nakadhalika.
                                   
                                                NUI/TANZU ZA NYIMBO
Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.

Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.

Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.
Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.

Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini.

Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi.

Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.
Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.

Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuomboleza.

Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.

Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini nakadhalika.

Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.

Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto.

Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.
Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.

Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.                

Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.
Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi.

Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.

Sifo; hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.

Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.

Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.  

Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.
Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.

Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.

Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.

Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.

Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.

FASIHI SIMULIZI NA FASIHI ANDISHI (FASIHI YA MAJARIBIO)
Katika mukitadha huu kuna mwingiliano wa tanzu za fasihi yaani fasihi simulizi na fasihi andishi. mwingiliano wa tanzu, fasihi simulizi ina kanuni zake zitumikazo katika kuambatana na kuamuliwa na utanzu huo. Kanuni ni mambo yanayojitokeza mara kwa mara katika utanzu huo. Fasihi andishi inachota baadhi ya mambo katika fasihi simulizi. Wataalamu wengi wa fasihi wanachota vipengele vya fasihi simulizi na kuvitumia katika uumbaji wa kazi za fasihi andishi. Na kanuni hizi zimewakuza watoto tangu enzi za vitendawili, fasihi simulizi fasihi mpaka itamkwe kwa mdomo.

KANUNI ZA MASIMULIZI
Ø      Uelezwaji na utambwaji
Ø      Sifa za mtambaji
Ø      Hadhira na nafasi yake katika uelezaji
Ø      Taswira na ishara
Ø      Mianzo na miisho ya kifomula
Ø      Marudio rudio
Ø      Taharuki
Ø      Ucheshi
Ø      Tanakali sauti
Ø      Kuingiliana kwa tanzu
Ø      Muundo
Ø      Majina ya wahusika


UTAMBAJI NA UELEZWAJI

Fasihi simulizi si fasihi mpaka imetumia mdomo katika uwasilishwaji wake na utambaji huu hutegemea sana aina ya hadhira. Mtambaji anaweza kutumia taswira kali na yenye kufikirisha kwa hadhira yenye elimu ya juu, pia matumizi ya misemo, na methali zaweza kutumika. Si kila mtu anaweza kuwa mtambaji mzuri bali kila mtu ni mtambaji. Mfano mtambaji hawezi kutumia taswira kali kwa watoto wadogo. “ sikia wanangu gagulo la bibi sasa linadondoka hadharani wala hakuna anayejaribu hata kumsaidia kulipandisha katika kiuno chake.
 
Imeandaliwa na: Kapele. H, 2013
                           TEKU/BAED/HK
                            Pia waweza kupata msaada wa mada mbalimbali katika
                            www.kapeleh.blogspot.com
                 KISWAHILI NI TUNU NA JOHARI YA AFRIKA




  
     
             


15 comments:

  1. asante sana wana blog kwa mambo mazuri kama haya. muendelee kutuletea zaidi na zaidi. by zacharia japhet teku/baed/hk/11886

    ReplyDelete
    Replies
    1. Unaharaka gani kaka? Kumbuka umuhimu wa uakifishi.

      Delete
  2. Kweli kiswahili ni TUNU, sio lazima mambo yote yanayotupiwa humu yawe ya lugha ya ya kigeni.
    NSYANI KISSA E.
    TEKU/BAED/HK/11833

    ReplyDelete
  3. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  4. JOHN PASCHAL TEKU/BAED/HK/11657
    Nimefurahi sana kwa harakati hizi za kutumia teknolojia kuelimishana sisi kwa sisi.

    RAI KWA UTAWALA WA BLOG HII
    Napendekeza uso wa blog hii uwe na vijisehemu ili kutenganisha maudhui yanayohifadhiwa humu. Kwa mfano TED, TLK, THT, Entertainment, News, etc. Ni mtazamo tu msinione msemaji sana- natumia Kiswahili!

    ReplyDelete
  5. hakika kiswahili kama maji usipoyanywa basi utayaoga

    MARO EMANUEL

    TEKU/BAED/HK/11727

    ReplyDelete
  6. facebook is social network which many people share their views and can be used both in the computer and phones while what sap can be used in the phone/

    ReplyDelete
  7. Hakika kiswahili hakina budi kupewa kipaumbele toka shule za awali mpaka ngazi ya chuo kikuu na kitumike katika masomo yote tuache kutukuza lugha ya watu. hongera Kapele kwa kutumia muda wako vyema na kutupatia vitu adimu katika lugha adimu ya kiwsahili.
    KANYANSA GIBSON TEKU/BAD/HK/11674

    ReplyDelete
    Replies
    1. ALFRED MAKIYA MUCE-BAED-Ps,Ksw2 May 2014 at 03:40

      Mungu awatangulie wanoifanya lugha ya kiswahili ijulikane duniani

      Delete
  8. safiii!, endelea hivyo hivyo utakua kama Shaban Robert

    ReplyDelete
  9. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  10. Mhume Fikiri TEKU/BAED/HE/11387
    Wadau,TED 501 tukomae maana mmmmmmmmmmm!

    ReplyDelete
  11. Ngependa kutao shukrani zangu za dhati kwa mchapishaji kwa kutueleza mambo mengi juu ya kiswahili. mimi ni mwanafunzi wa kiswahili chuo kikuu cha maseno, na ngependa kufafanuliwa kwa kina asante-kiprutoanthony@yahoo.com

    ReplyDelete
  12. asante sana,nimepat nilicho kiitaji

    ReplyDelete
  13. Mnafanya kazi nzuri, Lakini nawaombeni mjaribu kuchambua nadharia zinazotumika katika fasihi kwa undani zaidi ili tuweze kutambua kinagaubaga

    ReplyDelete

PRONS DJ D69

PRONS DJ D69
THE PRIDE OF TANZANIA

BLOGGERS

BLOGGERS