FASIHI SIMULIZI
M.M. Mulokozi (1996) anasema, Fasihi
Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira
kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.
TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya
fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia
ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na
vitendawili.
Baada ya kuangalia maana ya fasihi
simulizi yafuatayo ni maaelezo kuhusu chimbuko la fasihi simulizi kupitia
nadharia ya ubadilikaji taratibu ambayo itathibitisha kauli isemayo kuwa fasihi
simulizi ni masalia ya kazi au sanaa za vizazi vya kale. Kwa mujibu wa Okpewho, (1992)
anasema kuwa mwanzilishi wa nadharia hii ni Charles Darwin ambaye anasema kuwa
“viumbe hai vyote vimekuwa vikipitia mabadiliko mbalimbali ya muda mrefu hadi
kufikia hali hii tuiyonayo sasa”. Dhana
yake hii imeleta ushawishi mkubwa kwa wanataaluma mbalimbali wa fasihi simulizi
ambao wanaamini kwamba, fasihi simulizi ni masalia ya zamani au mabaki ya sanaa
jadi zilizotangulia kama vile visasili,
visakale, ngano, hekaya, methali, nyimbo, vitendawili nk.
Wanaendelea
kusema kuwa sanaa hizi zilirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na
ziliendelea kupoteza uhalisia wake kadri muda ulivyozidi kwenda. Nadharia hii
ilitawaliwa na mbinu ya ulinganishi ambapo walijikita zaidi katika kulinganisha
fasihi ya jamii moja na nyingine na katika ulinganishaji wao waliangalia zaidi
kipengele cha maudhui kuliko kipengele cha fani.
UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI
KATIKA JAMII
Licha ya
wanaubadilikaji taratibu kuonesha uhalisia wa fasihi simulizi kuwa ni masalia
ya kazi za kale au mabaki ya zamani, hoja hii haimaanishi kwamba fasihi
simulizi haina thamani au uamilifu wowote katika jamii ya leo lahasha! Hivyo
tunaungana na wanasosholojia ambao wanasisitiza kuwa uamilifu wa fasihi
simulizi upo hai ila unabadilika tu kulingana na maendeleo ya jamii husika na
dhima zake zinatawala masuala mtambuko kama
ifuatavyo:
Kuburudisha;
tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hutumika kama
nyenzo ya burudani katika Nyanja mbalimbali za kijamii. Mfano wa tanzu hizo ni kama vile hadithi, ushairi (nyimbo mbalimbali), semi
(methali, vitendawili). Tanzu hizi hutoa burudani katika sehemu mbalimbali,
mfano nyimbo, zipo nyimbo ambazo hutumika kutoa burudani katika sehemu
mbalimbali kama vile harusini-nyimbo za
harusi, nyimbo za nyiso hutoa burudani jandoni na unyagoni. Vilevile katika
siasa zipo nyimbo ambazo hutumika kutolea burudani na uhamasishaji wakati wa
kampeni za kisiasa. Hivyo basi kutokana na utanzu huu wa nyimbo kutumika kama chombo cha burudani katika Nyanja mbalimbali
huonesha dhahiri kuwa ni kwa namna gani fasihi simulizi inavyojitokeza katika
masuala mtambuko.
Kuelimisha;
kupitia fasihi simulizi jamii hujipatia elimu ambayo huwasaidia kuijua vizuri
historia yao, utamaduni, siasa ya nchi yao pamoja na itikadi.
Mfano katika historia zipo kazi za fasihi simulizi ambazo huonesha historia,
kazi kama utenzi wa Fumo Lyongo, utendi wa
Shaka Zulu ambao hutupatia historia na utamaduni wa watu wa Afrika kusini. Pia
ndani ya tendi hizo kuna masuala ya uongozi pamoja na siasa. Vilevile zipo
methali ambazo huelimisha watu kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea nafasi yao kiuchumi, kwa mfano;
“mgaagaa na upwa hali wali mkavu”. Kadhalika katika upande wa afya zipo methali
zinazotoa elimu mfano “kinga ni bora kuliko tiba”. Hivyo basi utoaji huo wa
elimu katika Nyanja tofauti tofauti huonesha ni kwa namna gani fasihi hii
ilivyokuwa inajihusisha na masuala mtambuko ya kijami.
Kuhifadhi
historia na utamaduni wa jamii; katika suala hili pia fasihi simulizi haikuwa
nyuma kwani zipo kazi mbalimbali ambazo hutumika kama nyenzo kuu na muhimu za
kuhifadhia amali za jamii kwa mfano visasili na visakale hutunza historia na
utamaduni wa jamii husika, mfano; kisasili cha kibo na mawenzi hutunza historia
ya Tanzania kuhusu mlima Kilimanjaro. Pia zipo methali ambazo hutunza utamaduni
wa waafrika hususani Tanzania
mfano; “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”, methali hii hutunza utamaduni wa
kiafrika kuwa wadogo lazima wawasikilize na kuwaheshimu wakubwa. Kadhalika
katika siasa kupitia kipera cha lakabu ya baba wa taifa huonesha historia ya
kiongozi wa Taifa la Tanzania.
Na hivyo ndivyo namna fasihi simulizi inavyojihusisha na masuala mtambuko.
Kuhamasisha
umoja na mshikamano; suala hili pia hufanywa na aina hii ya fasihi simulizi
katika jamii na hujidhihirisha katika Nyanja mbalimbali kama
vile siasa, zipo methali ambazo uhamasisha suala hili:- “Umoja ni nguvu
utengano ni udhaifu”, “Kidole kimoja hakivunji chawa”. Kwa upande wa nyimbo
zipo pia ambazo huhamasisha suala hili kama
vile nyimbo za chapuzo mfano; wawe-kilimo, kimai-uvuvi. Vileveli zipo nyimbo
ambazo huhamasisha umoja na mshikamano wakati wa michezo.
Kukuza lugha;
fasihi simulizi hujikita pia katika suala hili la ukuzaji lugha kupitia vipera
mbalimbali ambavyo hufanyika katika nyanja mbalimbali kwa mfano nyanja ya
elimu, vipo vipindi mbalimbali redioni na hata kwenye luninga ambavyo hutumika
kufundishia lugha hasa kwa watoto kwa kupitia vipera vya fasihi simulizi kama
vile vitendawili na methali, zipo pia chemshabongo na hadithi mbalimbali.
Vilevile ipo michezo ya watoto ambayo hukuza lugha kama
vile kauli tauria, mfano; “Katibu kata wa kata ya mkata alikataa katakata
kukata miti katika kata ya mkata”. katika siasa uibukaji wa misimu mfano,
chakachua, ngangari nk. pamoja na nyimbo hasa wakati wa kampeni husaidia kukuza
lugha. Pia shughuli mbalimbali za kijamii mfano harusi, misiba kupitia nyimbo
za watani pia hutoa mchango mkubwa katika kukuza lugha.
Kuonya na
kukosoa jamii zipo tanzu na vipera mbalimbali vya fasihi simulizi ambavyo
hujihusisha zaidi na kuiweka jamii katika nafasi iliyobora zaidi. Mfano;
kimaadili kuna methali zinazoonesha maadili mema katika jamii mfano; “Samaki
mkunje angali mbichi”, “Mkaidi hafaidi mpaka siku ya iddi”. Vilevile kiuchumi
zipo methali ambazo huonya na kukosoa wale wote wenye tabia za kivivu katika
kujitafutia maisha mfano, “Mtegemea cha ndugu hufa masikini”, “Fanyakazi kama
mtumwa uishi kama mfalme”.
Vilevile
kuongeza kipato; kupitia fasihi simulizi watu hujiajiri na kujipatia kipato.
Kwa mfano; watu hujishughulisha na utanzi wa nyimbo mbalimbali kama vile nyimbo za kisiasa, kiuchumi pamoja na nyimbo za
kiutamaduni ambapo kwa namna moja au nyingine huwasaidia katika suala zima la
kujipatia kipato na kusukuma mbele gurudumu la maisha kwa ujumla.
Masuala mtambuko ni mambo yanayojitokeza
katika Nyanja mbalimbali za kijamii, kwa mfano magonjwa, rushwa, ufisadi nk.
Mfano wa Nyanja hizo ni kama vile siasa,
uchumi, utamaduni na jamii kwa ujumla
TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea
au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa
na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia,
Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila (2003).
Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea
vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo,
vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)
Tanzu hizi za fasihi simulizi
huweza kuwekwa katika kumbo au michepuo yake. Bali
upo utata katika kuainisha kumbo hizi, utata huu uanasabishwa na kutokuwepo kwa
nadharia teule ambazo zingeweka wazi njia au vigezo muhimu ambavyo vingefaa
kutumika katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi. Katika kutalii uwanda
wa fasihi simulizi wataalamu wengi wanatumia vigezo vya maudhui, fani, matukio,
idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika, na namna ya uimbaji. Hebu tuyatalii
mawazo ya watalaamu hawa na uainishaji wa kumbo za fasihi simulizi.
Mulokozi (1996), mtaalamu huyu
yeye anajaribu kuainisha tanzu sita za fasihi simulizi ambazo ni:
a. semi
b. mazungumzo
c. masimulizi
d. maigizo
e. ushairi
f.
ngomezi
Ndungo na Wangali, wao
wanazianisha tanzu tano za fasihi simulizi wanaanza na:
a. hadithi
b. ushairi na nyimbo
c. sanaa za maonesho
d. methali
e.
vitendawili
wataalamu wote wanamitazamo
inayoendana katika kuainisha tanzu za fasihi simulizi, baada ya kutambua mawazo
yao sasa ni
vema kutumia nafasi hii kuziweka tanzu hizi katika makundi jumuishi manne ambayo
ni:
a. sanaa za maonesho
b. semi
c. masimulizi
d. ushairi
tanzu hizi zinahusiana katika
kukamilisha utendaji wa fasihi simulizi na ili kujadili vema ni vema tuanze na
mchepuo wa semi.
SEMI
Ni tungo au kauli fupifupi za
kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Katika kuainisha
utanzu huu vipo vigezo kama vile kigezo cha
lugha na kigezo cha dhima ambacho kujifunza.Tanzu au kumbo hili lina vijitanzu
vyake vinavyotumika katika kuweka uhai wake, nanvyo ni:
a. methali
b. vitendawili
c. mafumbo
d. misimu
e. lakabu
f.
kauli- tauria
Baada ya kujua
vijitanzu vya utanzu wa semi sasa ni vizuri kuanza kujadili kijitazu cha kwanza
ambacho ni methali, katika kijitanzu hiki tutajadili maana, chimbuko, umiliki,
uwasilishaji, muundo, mitindo, sifa, na umuhimu wake kwa jamii.
METHALI
Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo
mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii, au ni maneno ya hekima na busara ambayo hutolewa na mtu mmoja na baadaye
maana ya maneno hayo hutolewa. Jambo la msingi katika kutoa maana ama
fasili ya methali ni kuangalia mazingira. Pia
methali ni usemi mfupi wa mapokeo ambao hudokeza kwa ufupi tajiriba ya jamii fulani.
Chimbuko la methali
methali zinatokana na:
a.
visasili, mfano nyama
ya ulimi huponya imetokana na masimulizi ya Kiswahili yaliyomuhusu mfalme.
b.
maoni na uzoefu Fulani wa kihistoria mfano
keshokesho haikumuua mzungu.
c.
Uchunguzi wa vitu katika
mazingira, tabia na mienendo ya watu katika jamii. Mfano, moto hauvukwi mara
mbili. Methali hii huimiza utendaji.
Umiliki wake
Methali kama kijitanzu cha semi humilikiwa na jamii nzima
hata kama ilitolewa na mtu mmoja. Kwa ufupi
twaweza kusema kuwa ni mali
ya jamii nzima.
Uwasilishaji wake
Uwasilishaji wake hutegemea zaidi unaongea na nani?
Unaongea nini? mfano unaongea katika mazungumzo rasmi kama
vile hotuba, ibada au risala.
Muundo wake
Methali huundwa kutegemea jamii moja na nyingine na aina ya
maudhui. Mfano methali ya swali, mavi usiyala wayawangiani kuku?
Mla
mla leo mla jana kala nini?
Pilipili uso ila yakuwashia nini?
Methali muundo wa sentensi
a.
masikio hayazidi
kichwa
b.
mkate makavu wa nyumbani ni
bora kuliko nyama ya shuwa yap engine.
c.
Kata pua uunge wajihi
d.
Mwenda tezi na omo marejeo ni
ngamani
e.
Mwenda kwao si mtoro.
f.
Mwenda kwao haogopi giza.
Mtindo wa methali
Katika mitindo ya methali yapo
mambo muhimu yaliyoingizwa miongoni mwa mambo hayo ni:
- Sitiari zimeingizwa zaidi. Mfano ukiona vyaelea jua
vimeundwa, mgeni ni kuku
mweupe.
- mirudiorudio ya silabi au sentensi. Mfano ukiujua
huu, huu huujui, hayawi hayawi huwa.
SIFA ZA METHALI
Methali zina
sifa zifuatazo:
i.
zinaufupisho wa maneno
ii.
zina muundo wa kishairi.
iii.
Huingiza lugha ya
iv.
Hujulikana na jamii nzima
v.
Huwa na pande mbili (nyingi)
Katika kujadili
sifa za methali mtaalamu mmoja amejaribu kuzigawa methali katika makundi manne
(4), ambayo ni:
i.
Methali za imani ya binadamu kwa Mungu. Mfano, muumba
ndiye muumbua, Mungu ndiye muumba, kalamu ya Mungu haikosi.
ii.
Methali zinazo taja binadamu na viungo vyake. Mfano,
hawi Musa kwa kuchukua fimbo, ugeni ni utoto, usiwe na kucha ndefu.
iii.
Methali zinazotahamini matendo na tabia za watu (hujenga
tabia njema) mfano asiona nafsiye haoni akioneshwa.
iv.
Methali zinazotaja mambo au matendo mbalimbali
yanayotokea mara kwa mara na kuathiri maisha ya binadamu. Mfano, mtenda mema
kinyuki jaziye hulipwa mema, kenda fumbata si kumi nenda rudi, ndege
aliyemkononi ni bora kuliko kumi walio mtini, ajali inasababu.
UMUHIMU WAKE KATIKA JAMII
i.
Methali huelimisha jamii,
ii.
Methali huonya na kuhasa jamii
iii.
Methali hukuza uwezo wa kufikiri ( hufikirisha)
iv.
Methali hutunza amali za jamii husika.
v.
Methali hujenga mahusiano mema.
Methali ni utanzu unaotegemea sana fani nyingine ili
uweze kukua na kuenea, mfano maongezi au majadiliano mazito. Pia kipera hiki na
ni sanaa elezi kwa hutumiwa kufafanua na kukazia jambo linalozungumzwa ili
ieleweke vizuri. Mwisho methali inaweza kuwa na umbo au mtindo wa kishairi,
mfano haba na haba hujaza kibaba.
VITENDAWILI
Kama ilivyo katika methali utaratibu uliotumika kufafanua
kipera methali utatumika pia katika kufafanua kipera vitandawili.
Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa ambao
hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha lugha.
Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo. Pia vitendawili ni semi fupi
zenye kuwakilisha maana pekee za vitu, vitu vinaweza kuwa kimazingira au
kitabia, vilevile zinahitaji kuwa na maana sahihi za kifasihi. Mteguaji
anatakiwa ategue kifasihi na apate dhana inayotegemewa.
MAMBO YA KUZINGATIA
KATIKA VITEDAWILI
i.
Tatizo la kutatuliwa.
Kanuni ya utangulizi inapoanzwa.
ii.
Kitendawili si kitendawili
hadi kiteguliwe. Hivyo jibu ni sehemu ya kitendawili mwanzo wa kifomula, majibu
na hatua zote zinazofuata na majibu yanaposhindwa kuteguliwa ni kitendawili.
Mwanzo hadi mwisho ni kitendawili, kila hatua ni sehemu ya kitendawili.
Uainishaji
Fani na maudhui kifasihi hutumika. Uainishaji wowote ule
hutegemea vitu fulani katika maudhui kuna ujumbe, dhana…
Maudhui ni jumla ya mambo yote yanayosemwa katika maandishi ama
ktaika mazungumzo.
Fani hushughulika na kwa vipi kitu ama maudhui yanavyosemwa au
kuwasilishwa. Mtindo, wahusika na mtindo. Vifuatavyo ni vigezo vya uainishaji
wa vitendawili.
- Tukio au jambo. Katika kuelezea kigezo hiki
watu, wadudu, mimea, teknolojia,
mila na desturi
huusika. Mfano miti yote nipanda lakini mtalawanda utanishinda.
Jibu: huwezi
kumuoa dada yako.
- Urefu. Kuna urefu wa aina mbili: mpumuo
– moja (maelezo mafupi) mfano nyumba yangu haina mlango. Jibu yai,
mpumuo-
mwingi/ mrefu. Mfano kulikuwa na mama alikuwa na watoto
warefu…lakini bado kunautata katika vigezo hivi vya vitendawili. Hivyo
basi ni vema kikatumika kigezo cha ugumu au utata pamoja na kile cha
urahisi katika kuainisha vitendawili.
VITENDAWILI
TATA (SIFA)
i.
huanza na kanuni.
ii.
Huwasilishwa kwa
maneno yenye mtiririko na maswali.
iii.
Hufunguliwa na akili
na uwezo mkubwa.
iv.
Huwasilishwa…
VITENDAWALI RAHISI
(sifa)
i . huanza na kanuni ama fomula.
ii. ni sentensi wala si swali.
iii.
ni vya moja kwa moja
na hueleweka moja kwa moja.
iv.
Hutegwa kwa urahisi
kutegemea mkitadha na kunga za vichekesho na kishairi.
MTINDO AU MBINU ZA
VITENDAWILI
Kuna mitindo mingi ya vitendawili kama
ifuatavyo:
·
Onomatopia (matumizi
ya sauti ) mfano prii mpaka maka, fu funua.
·
Mbinu ya kishairi,
mpango wa maneno na mapigo ya kimziki. Mfano
futika futika futikafutika.
·
Matumizi ya nafsi na
uhaishaji. Mfano popoo mbili zavuka mto
·
Matumizi ya kejeli.
Mfano kitu kidogo kimemtoa mfalme kitini.
·
Matumizi ya tashbiha.
Mfano msichana mdogo anapika vizuri kuliko mama yake- nyuki. Babu mfupi
anamwangusha babu mrefu- shoka
UWASILISHAJI
Uwasilishaji wa vitendawili unategemea sana uwepo wa pande mbili ambazo ni: mtegaji-
anayetoa, mteguaji- anayejibu. Kuna mabadilishano na hakuna hadhira katika
uteguaji. Katika baadhi ya makabila wazee wanaweza kuwa hadhira kabla ya kutega
huanza na tangazo. Mfano tutaanza kutega na kutegua vitendawili.
KWA NINI KANUNI
KATIKA VITENDAWILI
Kuna umuhimu mkubwa wa kufuata kanuni katika vitendawili,
na umuhimu huu ni kama ifutavyo:
i.
Kuandaa utayari
kiushindani.
ii.
Kuwatoa washiriki
katika shughuli zao na kufuata mukitadha wa kiutendawili
iii.
Huwafanya washiriki
kuwa makini ….
iv.
Kufafanua na kuainisha
mtegaji na mteguaji katika kundi.
v.
Huwajulisha kitendawili
kinachofuata. Kwa kawaida vitendawili hutolewa na watoto au ni vya watoto.
Lakini haina maana kuwa watoto ndio wahusika wakuu. Mara nyingi hutegwa usiku.
Kwa sasa vitendawili husomwa shuleni, mukitadha wa vitendawili umebadilika
kutokana au kulingana na mabadiliko na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kuhama kwa vitendawili hubadulika maana.
UMUHIMU WAKE
i.
kufikirisha
ii.
kujenga umoja
iii.
kukuza na kuitunza
utamaduni
MAMBO YA KUZINGATIA
KATIKA UCHAMBUZI
- Muda au wakati ( muda gani kilitegwa na sasa kinategwaje)
- Mazingira. Mfano kuku wangu katagia mwibani- nanasi.
(zingatia mazingira)
- Maana na jibu litolewe. Mfano kaburi la mfalme lina
milango miwili.
- Matumizi ya lugha. Mfano chaka langu halina ubaridi. Ili kuelewa dhana za vitendawili tambua mazingira, silka,
na utamaduni wa watu.
Swali muhimu.
Vitendawili ni fasihi ya watoto, hivyo ni kupoteza muda
kuvisoma katika mihadhara ya chuo kikuu. Jadili.
Dondoo za
ujibuji.
i.
utangulizi
-
maana ya vitendawili
-
sifa za vitendawili
-
uwasilishaji wa
vitendawili
-
sifa za vitendawili
ii.
kiini
-
umuhimu wa kusoma
vitendawili kama kipera cha semi katika fasihi
simulizi.
iii.
hitimisho
- mambo ya kuzingatia katika uchambuzi wa vitendawili.
MAZUNGUMZO
Mazungumzo
ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote
lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na
usanii wa aina fulani. Mfano
wazungumzaji wanaweza kutumia lugha ya makato, methali,vitendawili, nahau, na
tamathali za semi katika kuzungumza kwao. Matumizi ya lugha ya kisanaa katika
mazungumzo hufanaya mzungumzo yakawa utanzu wa fasihi simulizi. Mazungumzo kama
utanzu wa fasihi simulizi una vyake vipera ambavyo ni: hotuba, soga, malumbano,
mawaidha na ulumbi.
Hotuba; haya
ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au
kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha
ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo
cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano
katika vikao rasmi au mikutano.
Soga;
haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake
ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha
inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake
huwa ni mahali popote.
Mawaidha; haya ni maneno ya
maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo
kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake
ni kuonya au kutoa muongozo.
Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala
uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au
mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo
cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha
wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.
Ulumbi;
huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha
iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.
Mawaidha;
haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo.
Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.
SANAA ZA MAONESHO – UTANZU WA
FASIHI SIMULIZI
Ni maigizo ya fasihi simulizi,
maigizo haya huusisha mambo ya dhati ya kutoka kwenye hali zao halisi katika
mapito ya maisha na kurudiwa kimchezo na vikundi vya waigizaji. Katika maonesho
lazima mtu aone lakini matendo huboresha zaidi. Fasihi simulizi ni halisi ya
mwafrika. Ingawa utanzu huu una mambo ya dhati una vipera vyake kadhaa ambavyo
ni: majigambo,maigizo, tambiko, miviga, michezo ya watoto, utani, ngonjera,
ngomezi vichekesho na michezo ya jukwaani. Vipera hivi vyaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:
MICHEZO YA WATOTO
Michezo hii hufungamana na
utamaduni na siasa ya jamii, ni msaada kwa watoto kujifunza mambo ndani ya
jamii. Washiriki ni watoto wenyewe, hata kama
mtoto yuko peke yake huumba wahusika wake akilini. Mfano mtoto kuongea peke
yake katika mchezo fulani. Pia watoto wengi hucheza michezo inayozuka katika
jamii yake. (kuiga, kutenda, kuona). Kisayansi ubongo wa watoto huzaliwa ukiwa
wazi na kila apokeacho ni sahihi. Michezo hii huchezwa popote na kila mchezo
huwa na shabaha na watoto huiga utamaduni wao na vifaa vinavyotumika ni vile
vinavyopatikana ndani ya jamii.
LENGO AU MADHUMUNI
i.
kuburudisha.
ii.
Kuelimisha/kufunza.
iii.
Kuonesha utamaduni.
TAMBIKO
Ni sadaka kwa Mungu, miungu au
mahoka kulingana na jami. Kwa nini tambiko: kuomba (mvua, magonjwa), kushukuru.
Katika tambiko yapo mambo muhimu yanayofanya tambiko liwe miongoni mwa vipera
vya sanaa za maonesho mambo hayo ni:
i.
uwanja wa kutendea,
mfano: miti mikubwa, njia panda, kaburi na misitu minene.
ii.
Maleba, hivi ni vifaa
maalumu ambavyo hutumika katika matambiko, mfano: ngozi, mashuka, mgwishu,
kisu, kibuyu.
iii.
Lugha maalumu. Katika
matambiko kuna lugha maalumu inayotumika., lugha hii ni lugha ya unyenyekevu,
utulivu na yenye utofauti mkubwa.
iv.
Utendaji katika
tambiko, huwahusisha viongozi, wafuasi na dhamira. Vitu hivi hutendwa na
kuzungumzwa.
MAIGIZO
Maigizo ni michezo inayotumia
watendajikuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine. Lengo kubwa ni
kuburudisha na kutoa ujumbe. Maigizo ya kiafrika kama
vile maigizo ya watoto, maigizo ya kidini, maigizo ya msibani huambatana na:
a. ngoma
- hadithi
- nyimbo
- matendo
ya kimila
- utambaji.
MIVIGA/ JANDO NA UNYAGO
Haya ni mafunzo yanayomfanza mtu
namna gani aweze kutenda yeye kama mtu mzima.
Unyago ni ngoma ya kumfundisha mwali katika jamii yake. Pia ni taasisi rasmi kama taasisi nyingine. Miviga hii ina zake sifa ambazo
ni:
i. utendaji, unaohusisha ngoma na
nyimbo.
MAJIGAMBO
Ni kujifanya unajua sana, kujinata na
kujivuna. Sanaa iliyokinyume na majisifu mara nyingi katika shairi na
masimulizi, mambo makuu na matukufu aliyowahi kuyafanya mtu fulani na mara
nyingi sifa za kiumeni hutumika, kuchezwa ngomani na katika masuala ya
kiserikali na waimbaji hutumia zeze.
UTANI
Mila ya utani imeenea sana Afrika. Watu wanao
taniana kwa maneno na matendo, masharti huzingatiwa. Malumbano ya utani yapo katika
michepuo mingi kama ifuatavyo:
i.
utani wa babu, bibi na
wajukuu.
ii.
Utani wa mashemeji.
iii.
Utani wa makabila.
iv.
Utani wa marafiki.
MASIMULIZI
Masimulizi; hii
ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu
huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika
katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha muundo,
mara nyingi masimulizi huwa na muundo.
katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.
Katika masimulizi muundo wake
mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vilevile
kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha
wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji. Pia kigezo kingine ni
kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na
msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa
maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na
uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika
muda maalum.
Masimulizi yamegawanyika katika
tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi
(za kubuni) na tanzu za kisalua
(kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano.
Ngano
(vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu
maisha. Pia ngano ni masimulizi ya kubuni yenye kutoa mifano ya binadamu na
matatizo yake ulimwenguni na akili ya binadamu kutatua matatizo ili maisha yawe
bora zaidi japo kwa muda mfupi hapa duniani. Mafano wa ngano ni pamoja na abunuasi, sungura. Tena masimulizi haya husisitiza kuwa binadamu wajinga au
legevu wasiopenda kutumia akili katika kutatua matatizo hufikwa na matatizo na
wakati mwingine hufunzwa na ulimwengu. Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano
ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha
ya kinathari, kigezo cha dhima
ambacho huelezea au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine
kilichotumika ni kigezo cha wahusika
ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha vijipera
vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.
Dhamira kuu ya ngano huwa ni
maisha, kuelimisha roho mbaya, kutia moyo. Ngano hizi kwa kawaida huwa na
kianzio na kiitikio chake. Mfano, kianzio chaweza kuwa paukwa/hadithi!hadithi!,
pia kiitikio chake chaweza kuwa pakawa, au hadithi njoo! Utamu kolea.
Maudhui katika ngano yanaweza
kujikita katika mambo yafuatayo:
-
binadamu wajinga
hupata shida.
-
Utamaduni wa jamii
husika huonekana katika ngano.
-
Binadamu anaweza
kufanya vitu visivyowezekana katika dunia halisi.
WAHUSIKA KATIKA NGANO
Wahusika katika ngano wanaweza
kuwa:
- binadamu
tu
- binadamu
na wanyama.
- Binadamu
na pepo.
- Binadamu
na zimwi.
- Binadamu
na miti au mawe.
Uhusika mkuu ni wa binadamu kwa
yeye ndiye anayepata funzo. Katika muktadha watoto au watu wazima ambao
huchorwa tofauti, mfano mdogo wa umbo akili nyingi. Katika hadithi wanyama
hutumika kukejeli na kuelezea uovu. Mfano:
i.
kinyonga – mtu mwenye
tabia ya kubadilika badilika.
ii.
Simba- mtu mwenye
nguvu.
iii.
mkizi- mtu mwenye
tabia ya kulala sana
na asiyetambua lolote. Wanyama wadogo
huwakilisha wanyonge lakini hushinda.
USIMULIZI
WA NGANO
Usimulizi
au masimulizi ya ngano huwa ni changamano na huweza kuwa wa moja kwa moja na
kueleweka kwa maudhui kwa tegemea sana mwanzo hadi mwisho wa hadithi. Nyimbo,
mahojiano, na ngoma hubeba maudhui ya hadithi.
FANI YA
NGANO
Fani ni
namna mambo au maudhui yanavyosemwa na msimulizi au mwandaaji wa maudhui.
Katika ngano fani hujikita zaidi na matumizi ya:
Taswira,
jazanda, tashibiha, chuku
sambamba na tanakali sauti ambazo huzua picha akilini mwa
msikilizaji. Taswira inapokosekana wasikilizaji hupotelewa na mkondo wa hadithi
na kushindwa kuunganisha vitushi. Sifa yake kuu ni kwamba huwa fupi na kufanya
kusikika vizuri au rahisi.
VIPERA
VYA NGANO
Ngano
na vipera vyake ambavyo ni:
1. NGANO
ISTIARA: hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha
maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni
kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Kwanini mafumbo ilikuepuka
migogoro baina ya mtunzi ama msimulizi wa hadithi hiyo na wanajamii wanaoweza
kuhisi kuwa masimulizi hayo yanawagusa ama kuwahusu kabisa. Mfano kusadikika.
MBAZI: hii
ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama
kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika
kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima. Mfano mzuri ni hadithi ya Binti na
Chura.
KISA: hii ni hadithi fupi ya
kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima.
Na mara nyingi lugha yake huvutia.
2. VISAULA/
HADITHI ZA KIHISTORIA
Ni hadithi zenye kutoa historia
lakini si zote huwa za kweli nyingine hubuniwa. Utanzu huu umegawanyika katika vipera
vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.
VISAKALE/visakalo: haya
ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa. huchanganya
chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo).
Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia
yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.
MAPISI: haya ni maelezo ya kihistoria
bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho
huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli. Mfano miradi bubu ya wazawa.
TARIHI: haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe
zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea
matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji
ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.
KUMBUKUMBU: haya ni maelezo ya matukio
muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha
fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha
wahusika ambao ni watu.
VISASILI: hiki ni kipera kinachofungamana
na imani za dini na mizungu ya kijamii, pia hizi ni hadithi za kale zenye
kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na
maisha yao.
Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.
VISAINI:
haya ni masimulizi ambayo hueleza viini au chimbuko la watu fulani, chanzo cha
matukio yanayokanganya akili ya binadamu. Mfano: kifo, kuzaliwa, pia husimulia
mambo ya ajabu na imani za kidini na jamii husika. Visaini hivi vinafafanua
kuwa kifo ni adhabu toka kwa Mungu tena hupunguza huzuni na kuvikubali vifo.
3. KHURAFA/KHARAFA/HURAFA
Hizi ni
hadithi ambazo wanyama wamehusishwa zaidi/kwa wingi na kupewa tabia za
wanadamu, huwakilisha vitendo na lugha za binadamu. Mfano: sungura, simba, fisi
na kobe. Katika
hadithi hizi fanani huongea bila kuudhi watu au hadhira. Hivyo yampasa kutumia
lugha mficho ndani ya wanyama ili hadhira wasitambue nani anayesemwa. Umuhimu
wa masimulizi haya ni kuwa huifadhi utamaduni wa jamii. Ulimwengu wa wanyama katika
kharafa ni ulimwengu halisi wa binadamu. Na kawaida yake wanyama wadogo
huwashinda wakubwa.
4. HEKAYA
Hizi ni
hadithi ndefu kiasi ya mapokeo yenye kuzingatia matukio machache ya kusisimua
na kustajabisha. Inatambulika kwa ujanja wa muhusika mkuu. Aghalabu muhusika
anaweza kuwa mtu ama mnyama. Muhusika mkuu hujikuta katika mikasa mingi ni kana
kwamba ulimwengu mzima umejaa mikosi na kuonesha kuwa atangamia, hadi mwisho wa
kisa ndipo kwa maajabu kabisa aweze kuibuka mshindi na hii huifanya hadithi
kuwa na taharuki. Mfano: kisa cha bwana MSA, mzimu wa watu wa kale. Hadithi
hizi za hekaya ni visa vingi lakini muhusika ni mmoja. Mfano ABUNUASI, huko Ghana hadithi za aina hii huitwa ANANSE, Afrika zinaitwa BUIBUI, na huko Nigeria zinaitwa KOBE
dhamira kuu ni kuhimiza watu
wasife moyo na funzo katika hekaya ni kwamba ukubwa si hoja katika ulimwengu
wenye matatizo. Ukubwa wa akili ni ufunguo wa maisha.
5. MIVIGHA
Ni hadithi ambazo zikitiwa katika
mizani ya kisayansi, kihistoria na kiamumbile hazioneshi ukweli wowote.
Waliozitunga huisisha na vizazi vyao vichanga na matukio hayo huonekana na
kuaminika kuwa ni kweli yalitokea. Hadithi hizi huusu chimbuko la kabila ambapo
huamini kama kuna mwanzilishi na watu wote
huwa wana wa huyo. Huonesha imani ya watu katika jamii, inaambatana imani na
itikadi katika jamii.
6. MIGHANI
Ni hadithi zinazohusu mashujaa,
mashujaa hao huwa ni wa kitaifa na hustawi sana. Na huitwa majagina au jagina.
Hushughulikia sana
haki za watu na huwa watu wema. Huwa na wakinzani wao hao huitwa
majahili/jahili wao hawajali maslahi ya wengi, makatili, wakandamizaji na
katika hadithi hizi mpaka kati ya ukweli wa kihistoria na kibunifu hautambuliki,
mpaka sasa jamii zinaamini. Kunapokuwa na mapambano…..
Sifa za mighani:
i. Zina mfumo wa kimaigizo.
ii. Zinatumia ishara.
iii. Zinatumbuiza.
iv. Zinaufaraguzi wa maneno.
v. Zina mwisho maalumu.
vi. Kuna kuwa na fanani.
vii. Kuna utendaji.
viii. Huendana na mazingira.
NADHARIA
Kuna nadharia nyingi zitumikazo
katika fasihi simulizi nazo ni:
i.
Nadharia ya mgeuko/
mabadiliko.
Nadharia hii na
waasisi wake hudai kuwa fasihi simulizi huakisi fani ya wakati husiku. Asili ya
binadamu ni sawa jamii zote, jamii hizi zina maendeleo yanayofanana hata kama mazingira ya kijiografia yanatofautiana. Msimamo wao
wanamabadiliko ua mgeuko wanadai dhana ya kimsingi inayounganisha tamaduni zote
zinafanana, vionjo, ubunifu wa mawazo au fikra na imani. Hadthi moja inaweza kusimuliwa
jamii moja pia na jamii nyingine kwa utofauti.
ii.
Nadharia ya msambao.
Hii ni nadharia
ambayo wanamsambao wanasisitiza mahusiano yaliyopo kati ya jamii tofauti kwa
kuthibitisha kuwa kuna mahusiano ya kijiografia na kihistoria. Hadithi
zinafanana katika kila jamii. Zote bila mawasiliano yoyote. Na hadithi
husimuliwa kulingana na utamaduni husika. Waasisi wa nadharia hii ni THEODOR
BENFEY, EMMANUEL COSQUIN, JULIUS, KEARLE KROHN. Wanamsambao husisitiza zaidi
uhainishaji na muundo wa…..ni jamii yenye mfumo wa mawazo aina moja na si
mkinzano wa mawazo.
iii.
Nadharia ya kiutendaji.
Katika nadharia
hii kuna waasisi kama vile Bron Slawn,
Malinowski, Raddife Brown. Wao wanadai kuwa shughuli za kiutamaduni huzingatia
falsafa ya jamii. Jamii huchota masimulizi katika desturi, imani, ibada na
zimeegemea katika muundo zilizojiwekea.
iv.
Nadharia ya utendaji
mpya.
Waasisi wake ni
Raymond Firth na Edmund Leach. Wao wanadai kuwa jamii haina muundo mmoja bali
siku zote inamafarakano. Katika mtazamo wao jamii haiwezi kuzuia mafarakano. Ili jamii iweze kukua lazima mafarakano yawepo, hakika
jamii haiwezi kuwa sawa.
v.
Nadharia Umbuji.
Mwasisi wake ni
Vladimir Prop. Yeye anadai kuwa kuna mahusiano ya masimulizi na wahusika katika
kutengeneza msuko au mtiririko. Na anangalia jinsi hadithi zinavyoingiliana
katika msuko, mpango na utaratibu.
vi.
Nadharia ya Umuundo
Mwasisi wake ni
Cloude Levi, yeye anadai kuwa utamaduni unajumuisha vitu vinavyofanana
alichunguza visasili na kusema vinatumika kuelezea na kutatua matatizo. Visasili
ni hadithi za kweli zinazoelezea falsafa ya jamii husika na vinahusika na
maisha ya jamii.
UAINISHAJI WA
MASIMULIZI
Masimulizi
yanaweza kuainishwa kama ifuatavyo:
i.
Kimtiririko, msambao wa masimulizi kijiografia na
kihistoria. Mfano hadithi za vitu, matambiko/ibada, kuanguka kwa shujaa.
ii.
Kimaudhui, zinagawa masimulizi kulingana na ujumbe
ndani ya hadithi.
a.
Visasili vya imani za kishirikina, imani za kidini
kitamaduni. Mfano asili ya mtu na vitu.
b.
Ngano na Hekaya, ni masimulizi ya kihistoria na
kumbukumbu za mashujaa.
c.
Ubunifu na kufikirika, istihala hekaya za kufunza,
maadili ngano fupi za kubuniwa, kauli za uongo na za kubuni, hadithi za
mafumbo. Ngano, hekaya, visasili zinasimuliwa kuwa ni hadithi za kweli na
hazibadiriki.
iii.
Kijamii, zina makundi yafuatayo:
a.
kisiasa, mahusiano ya uongozi na
b.
kiukoo, zinahusu muundo wa familiya fulani. Mfano,
ndoa.
c.
Kidini, kunakuwa na uwepo wa mvua.
d.
Kimaadili, ulafi, ujinga,kukosa mtazamo, wizi.
e.
Kiuchumi, kuchukua na kukopa.
iv.
Tabia, zinahusu muhusika mkuu katika hadithi.
Mfano visa janja.
a.
hadthi za binadamu, muhusika-binadamu.
b.
Hadithi za wanyama, muhusika-mnyama.
c.
Hadithi za mizimu, muhusika-mzimu.
d.
Hadithi za jinamizi, muhusika-jinamizi.
e.
Hadithi za miungu, muhusika- matukio ya kiungu na
miungu.
f.
Hadithi za vitu visivyo na uhai- miti, mawe.
V.
kiutamaduni, unagawa masimulizi kuhusu kujamii na
kiutamaduni,
lakini pia uainishaji wake unahusu….
MUUNDO NA MTINDO WA MASIMULIZI
Kaka suala la uwasilishaji yapo
mambo muhimu ya kuangalia ni nani, wapi, kwa vipi hadithi inasimuliwa. Kuna
mitindo todauti ya masimulizi lakini kuna mfanano wa mwanzo-kati-mwisho.
Mwanzo- mwanzo wa hadithi una
kanuni zinazofuatwa na kiala jamii ina mwanzo wake. Mfano katika Kiswahili
mwanzo waweza kuwa hadithi! Hadithi! Pia paukwaa!
iv.
msimulizi na wasimuliwaji
v.
mahali au jukwaa la masimulizi.
vi.
Muda au wakati usiingiliane na shughuli nyingine za
uzalishaji mali.
vii.
Urefu wa hadithi.
viii.
Shughuli na mipaka yaa uwasilishaji. Hadhira ina amini
nini na kwa wakati gani, kwa nini hadithi hazisimuliwi mchana? Hadithi
hutegemea sana
ujumi wa jamii husika.
Usimulizi wenyewe, katika kipengele hiki kuna msimulizi,
masimulizi na hadhira.
Utanzu mwingine wa Fasihi
Simulizi ni ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa
hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya
kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani,
lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.
Katika utanzu huu kuna vipera
viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;
Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni
kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji,
muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno
yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia hadhira
inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada,
kilio nakadhalika.
NUI/TANZU ZA NYIMBO
Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo
umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita,
nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio
mbalimbali kama vile ngomani au harusini.
Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha
watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika
matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.
Bembea;
hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha
kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.
Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga
mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni
kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum
yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.
Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au
miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu
Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika
muktadha wa kidini.
Wawe;
hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo
huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake
ni kuchapusha kazi.
Tenzi;
hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni
kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.
Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za
masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha
kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa,
pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.
Mbolezi;
hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa
kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa
maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima
yake ni kuomboleza.
Kimai;
hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni
kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo
cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.
Nyiso;
hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo
kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira
maalumu, kama vile porini nakadhalika.
Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo
muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika
au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.
Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika
ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya
watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake
huwa ni watoto.
Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji
wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha
wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo
cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.
Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo
za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima
ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.
Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi,
useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa
uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo
kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha
kazi.
Maghani;
hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa
mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya
ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo
vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.
Kipera hiki kina vijipera vitatu
ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi.
Maghani ya kawaida ni
kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi,
dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.
Sifo; hizi ni tungo za
kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au
kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha
wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni
muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu
muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi
na tondozi.
Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na
muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni
lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile
sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha
wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha
muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya
muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na
masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya
utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.
Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi
pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama
na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba.
Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo
hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika
kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika
kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia
hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji
huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.
Ghani masimulizi ina vipera vinne
ambavyo ni rara,
ngano, sifo na tendi.
Rara ni hadithi fupi
nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika
kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika
kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo
ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha
wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.
Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya
kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa
uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani
masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa
uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi
wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.
Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya
mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa
kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya
kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa
papo kwa papo.
FASIHI SIMULIZI
NA FASIHI ANDISHI (FASIHI YA MAJARIBIO)
Katika
mukitadha huu kuna mwingiliano wa tanzu za fasihi yaani fasihi simulizi na
fasihi andishi. mwingiliano wa tanzu, fasihi simulizi ina kanuni zake
zitumikazo katika kuambatana na kuamuliwa na utanzu huo. Kanuni ni mambo
yanayojitokeza mara kwa mara katika utanzu huo. Fasihi andishi inachota baadhi
ya mambo katika fasihi simulizi. Wataalamu wengi wa fasihi wanachota vipengele
vya fasihi simulizi na kuvitumia katika uumbaji wa kazi za fasihi andishi. Na
kanuni hizi zimewakuza watoto tangu enzi za vitendawili, fasihi simulizi fasihi
mpaka itamkwe kwa mdomo.
KANUNI ZA
MASIMULIZI
Ø
Uelezwaji na utambwaji
Ø
Sifa za mtambaji
Ø
Hadhira na nafasi yake katika uelezaji
Ø
Taswira na ishara
Ø
Mianzo na miisho ya kifomula
Ø
Marudio rudio
Ø
Taharuki
Ø
Ucheshi
Ø
Tanakali sauti
Ø
Kuingiliana kwa tanzu
Ø
Muundo
Ø
Majina ya wahusika
UTAMBAJI NA UELEZWAJI
Fasihi simulizi si fasihi mpaka
imetumia mdomo katika uwasilishwaji wake na utambaji huu hutegemea sana aina ya hadhira. Mtambaji
anaweza kutumia taswira kali na yenye kufikirisha kwa hadhira yenye elimu ya
juu, pia matumizi ya misemo, na methali zaweza kutumika. Si kila mtu anaweza
kuwa mtambaji mzuri bali kila mtu ni mtambaji. Mfano mtambaji hawezi kutumia
taswira kali kwa watoto wadogo. “ sikia wanangu gagulo la bibi sasa
linadondoka hadharani wala hakuna anayejaribu hata kumsaidia kulipandisha
katika kiuno chake.
Imeandaliwa na: Kapele. H, 2013
TEKU/BAED/HK
Pia waweza kupata
msaada wa mada mbalimbali katika
KISWAHILI NI TUNU NA JOHARI YA
AFRIKA